Inasikitisha Risala ya Mtoto wa kike Zanzibar

 











Risala ya watoto iliotolewa siku ya maadhimisho ya mtoto wa kike Duniani tarehe 07 Oktoba,20201

 

Asalamu Alaikum.

Ndugu Waalikwa Mliohudhuria katika Maadhimisho haya ya Mtoto wa kike,  hatuna budi kumshukuru Mwenyezimungu kwa kutukutanisha hapa katika siku hii adhimu na tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwenu nyote mliohudhuria hafla hii, pamoja na taasisi zilizoanda zikiwemo Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Zanzibar Gender Coalition (ZGC), Umoja wa Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Kijiji cha Watoto SOS na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA –ZNZ) na wote mlioshiriki kwa namna moja au nyengine kufanikisha siku hii muhimu kwetu.

Ndugu mgeni rasmi na wageni waalikwa wakati Dunia inaadhimisha siku hii adhimu ambayo Mnamo Desemba 19, 2011, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitangaza Oktoba 11 kuwa siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike kwa lengo la kutambua haki za wasichana na changamoto za kipekee ambazo wasichana wanakabiliwa nazo ulimwenguni, na Zanzibar inaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku hii.

Wakati leo tunaadhimisha siku hii muhimu  visiwani hapa bado baadhi ya wanajamii wamekua na  uelewa mdogo au kwa makusudi wameshindwa kutambua  umuhimu wa nguvu ya mtoto wa kike kwenye jamii na badala yake wapo wanaoendelea kuamini kuwa mtoto wa kike si sehemu ya watu muhimu na tumekuwa  na  masikitiko na kilio cha muda mrefu tuanachokabiliana nacho ikiwemo matukio ya udhalilishaji wa kijinsia.

Ndugu mgeni rasmi kwa masikitiko makubwa yanayoendelea kuzitesa na kusononesha nyoyo zetu wakati leo hii sisi tunakutana hapa na kuadhimisha siku hii taarifa za kina zinaonesha kuwa kutoka Mwezi Januari hadi Agosti mwaka huu  jumla ya matukio 838 ya udhalilishaji yameripotiwa katika vituo mbali mbali vya Polisi Unguja na Pemba huku watoto wa kike wapatao 567 sawa na asilimia 68 wameripotiwa kubakwa na kesi hizo zipo katika hatua mbali mbali.

Taarifa za matukio haya ni dhahiri kuwa mtoto wa kike bado hayuko salama na anahitaji ulinzi wa kina kwa kila mmoja wetu ili kumkinga na janga hili ambalo miongoni mwa matukio yake ni athari pia za kisaikolojia na kupelekea wengine kukatisha kabisa ndoto zao za kusoma na kuwatalamu bingwa wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. 

Sisi watoto wa kike bado tunaendelea kuamini kuwa umuhimu wa ulinzi  kwa watoto wa kike ni jambo lisilopingika kwani iwapo ulinzi imara utafanyika ni chachu ya maendeleo kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

Ndugu mgeni rasmi tukizungumzia kuhusu hali halisi ya changamoto za kisheria Zanzibar wanaozokumbana nazo watoto wa kike badhi ya vipengele bado vinahitaji marekebisho kwa lengo la kupunguza ama kumaliza kabisa changamoto hizo ikiwemo matukio ya udhalilishaji wa kijinsia.

Kwa mfano licha ya uwepo wa Sheria ya ushahidi kwa mfumo wa elektroniki katika sheria lakini bado utekelezaji wa sheria hio umeshindwa katika Mahakakama zetu tofauti kwa madai ya kukosekana kwa vifaa ambavyo vingeweza kusaidia utekelezaji wa sheria hio,na kurahisisha watendaji wa matukio hayo kutiwa hatiani kwa urahisi zaidi.

Pia imezoeleka na kuonekana kuwa ni jambo la kawaida kesi nyingi za udhalilishaji kuchukua muda mrefu kukusanya ushahidi hivi sasa si ajabu kuona Mahakama na vyombo vyengine vikikusanya idadi kubwa ya kesi za udhalilishaji kwa zaidi ya miezi sita  wakidai kuendelea na ushahidi na hatimae kesi hizo huishia kufutwa kabisa na kusababisha familia kukosa imani na vyombo hivyo ama baadhi ya watendaji wa taasisi hizo.

Wakati haya yote yanafanyika Zazibar hivi sasa imekua kawaida kila siku  kupitia vyombo vya habari kusikia taarifa za watoto wa kike kubakwa na chakushangaza  zaidi baadhi ya wanaofanya haya wanaendelea kudunda mitaani na wengine kujisifia kwa madai ya kutofanywa lolote lile.

Ndugu mgeni rasmi nisingependa kueleza hili kutokana na  machungu ambayo yananifanya kukumbuka lakini hatuna budi kueleza kwa lengo la kuonesha uhalisia wakati leo tunaadhimisha siku hii, wapo baadhi ya watoto wa kike wenzetu waliofanyiwa unyama kwa nyakati tofauti na kuwasababishia majeraha yasioweza kufutika akilini mwao na kupelekea kuachana kabisa na masomo na hadi sasa wamekua wahanga  walio salia majumbani mwao huku wakipoteza kabisa muelekeo wa maisha,hakika inasikitisha.

Ndugu mgeni rasmi na wageni waalikwa sisi watoto wa kike tunaamini ulinzi salama dhidi yetu ndio njia ambayo itatupelekea  na kutufanya sisi kushika nafasi mbali mbali za uogozi kwa kuwa ushiriki wa wanawake kweye nafasi hizo ni jambo lisiloepukika kwa sasa.

Ndugu mgeni rasmi na wageni waalikwa,sisi  sote leo ni mashahidi  hapa jitihada na ufanisi unaooneshwa na Rais Samia Samia Suluhu Hassan  hivi sasa ni matunda ya nguvu kazi iliowekwezwa kwake na kupitia wanaharakati sambamba na  fursa mbali mbali ambazo aliwahi kupatiwa na kufanyika kazi.

Hivyo tunaamini kati yetu wapo watoto wengi ambao  wakifikisha umri wa kushika nafasi za uongozi  wanaweza kuwa kama Rais Samia au hata zaidi yake kiutendaji iwapo mazingira rafiki ya kuwawezesha wanawake kushika nafasi ya uongozi yatakua rafiki kwa wote.

Ndugu mgeni rasmi na wageni waalikwa wote mliohudhuria katika maadhimisho haya ningependa kutoa wito kwa watoto wenzangu majumbani kuongeza kasi ya kusoma na kutokaa kimya pale wanapokata na changamto tofauti wakiamini kuwa kukaa kimya si suluhisho ya matatizo yao badala yale tunapaswa kutoka na kupaza sauti zetu kupamba na adui aliedhamiria kuharibu maisha yetu tukiamini kuwa sisi watoto wa leo ni viongozi bora wa kesho.

Hata hivyo tungependa kuendelea kuwaomba nyinnyi wanaharakati na Serikali kwa jumla kutotuacha mkono na  endeleeni kutusimamia mukiamini kuwa bado tunahitaji kusaidiwa ili tuweze kutimiza malengo yetu,kwa maslahi ya Taifa kwa ujumla.

Na kwapamoja tunapaswa kutambua kuwa Nguvu ya mtoto wa kike inapatikana kwa mifumo bora,sheria imara na kushika nafasi za uongozi.

 

 

                               Ahsanteni kwa kunisikiliza.

 


About mmedia

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment