Baadhi ya Wanachama
wapya waliojiunga na chama cha ACT wazalendo wakionyesha kadi zao kijiji cha
Uzi Ng’ambwa Mkoa wa Kusini Unguja ambapo zaidi wanachama wapya 50 walijiunga
na chama hicho UNGUJA |
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo, Othman Masoud
Othman, amesema ili kuyafikia maendeleo ya kweli, kuna haja ya kuiongoza nchi
kwa misingi ya kistaarabu, inayojali matakwa na maslahi ya umma.
Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar,
ameyasema hayo leo akiongea na wafuasi na wanachama wa chama hicho, wa vijiji
vya Uzi na Ng’ambwa, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema Zanzibar itaweza kuendelea kwa kuzingatia mfumo bora na
makini, unaoheshimu misingi imara ya uongozi, ambayo daima inajali heshima utu
wa wananchi wake.
Othman ameitaja misingi hiyo kuwa ni pamoja na Katiba
inayohitajika sambamba na mfumo bora wa kusimamia na kutekeleza chaguzi huru na
za haki, zinazopelekea viongozi waadilifu.
“Kinachohitajika ni mfumo uliojengwa na misingi makini ya
uongozi na usimamizi wa haki pamoja na uwajibikaji, tukielewa kwamba uchaguzi
ndio msingi wa uwajibikaji”, amesema Othman.
Aidha amesema heshima ya Zanzibar ni ya tangu zamani, na kwamba
ilidhoofika, bali kwa sasa kunahitajika ari, ujasiri na uvumilivu wa hali ya
juu kuitetea, kuipigania na kuirejesha.
Ametolea mifano nchi za Singapore na Sychelles zilizosonga mbele
kimaendeleo na zinazowiana na visiwa vya Unguja na Pemba kijeografia, huku
akitaja heshima ya Zanzibar katika mahusiano ya mwanzoni kabisa ya kidiplomasia
ambapo Mataifa Marekani na Uingereza yalitanguliza Balozi zao hapa katika miaka
ya 1837 na 1841.
Amesema pamoja na mambo mengine yakiwemo uzuri na utajiri wa
asili uliojengeka kwa mila, silka na utamaduni bora, lakini visiwa vya Unguja
na Pemba vimejaa raslimali muhimu, bali zinazowanufaisha wageni, huku wananchi
wengi wakiendelea kuteseka na maisha duni.
Pia Othman ameeleza nia ya Serikali ya Awamu ya Nane kukabiliana
na changamoto zinazowakabili wananchi wa kisiwa cha Uzi, zikiwemo ukosefu wa
barabara, pembejeo za kilimo, bei isiyokidhi ya zao la mwani, na mapungufu
katika huduma za kijamii ambazo ni pamoja na elimu na afya.
Mheshimiwa Othman ametoa wito kwa wananchi kuendelea
kushirikiana na kuungamkono juhudi za kujenga misingi ya Serikali ya Umoja wa
Kitaifa ya Zanzibar, chini ya maridhiano ya kisiasa ambayo ni alama ya imani na
amani, ili kuiendeleza nchi.
Akijibu baadhi ya hoja za wananchi juu ya changamoto
zinazowakabili, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Omar Said
Shaaban, amesema Wizara yake inaandaa mazingira ya kuwaendeleza wananchi hao,
kwa kuhakikisha kunakuwepo mipango ya kuwapatia unafuu pamoja na juhudi za
kuongeza bei na ubora wa zao la mwani linalolimwa kwa wingi kisiwani humo.
Awali baadhi ya wananchi wameeleza changamoto zinazowakabili na
kubainisha namna walivyochoshwa na ahadi za muda mrefu za kuwapatia huduma muhimu
zikiwemo za ujenzi wa barabara inayokiunganisha kisiwa hicho, ambazo wamedai
hadi sasa hazijatekelezwa.
“Tumechoka kujenga barabara kwa mikono, na hiki ni kilio chetu
cha muda mrefu kwa kila kiongozi anayekuja lakini bado hatujapatiwa ufumbuzi”,
alisema Bi Fatma Mussa wa Uzi-Mwanzo, akiwasilisha changamoto ambayo
imekaririwa pia na Bi Masika Mansab wa Uzi Ng’ambwa mbele ya Mheshimiwa Othman
alipoongea na wazee wa kisiwa hicho.
Ziara hiyo imemjumuisha Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo,
Ismail Jussa Ladhu ambaye amewataka wananachama na wafuasi wa chama hicho
kuendelea na msimamo thabit wa kupigania hadi kufanikisha mamlaka kamili ya
Zanzibar bila ya kutetereka.
Viongozi mbali mbali walijumuika katika ziara hiyo ambao ni
pamoja na Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Salim Abdalla
Bimani, Wakurugenzi, Wenyeviti wa Mikoa na Wajumbe wa Kamati Kuu ya Chama
hicho.
0 Comments:
Post a Comment