WAKULIMA WA KILIMO CHA MCHAICHAI PEMBA WALIJIA JUU SHIRIKA LA ZSTC

 


Mmea wa mchaichai


WAKULIMA wa kilimo cha mchaichai kisiwani Pemba wamelalamika shirika la Biashara la ZSTC kuwashushia bei ya mafuta ya mchaichai, licha ya kuwa soko la bidhaa hiyo liko pale pale.

Wakizungumza na waandishi wa habari wakulima hao walisema, kinachowashangaza ni kwamba soko la mafuta ya mchaichai halijashuka, ingawa wakulima wameshushiwa bei kutoka 200,000 hadi kufikia 120,000 jambo ambalo limewatia hasara kubwa.

Walisema kuwa, ipo haja kwa ZSTC kuwaangalia kwa jicho la huruma wakulima hao, kwani wamekuwa wakifanya kazi kubwa huku wakiajiri vijana wa kuwasaidia, ingawa kwa sasa wameshindwa kurudisha hasara na kushindwa kuwalipa wasaidizi.

“Kwa kweli tumeingiwa wa ugonjwa wa shinikizo la damu (presha) kwa sababu tumeajiri vijana ili tuwalipe baada ya mavuno lakini matokeo yake kwa bei tuliyopangiwa kuwauzia ZSTC hatupati kulipa gharama tulizotumia na wala hazikidhi kuwalipa vijana hao, ni mtihani kwetu”, walisema wakulima hao.

Walieleza kuwa, katika soko la kimataifa lita moja ya mafuta ya mchaichai wananunua shilingi 320,000 ingawa shirika linanunua kwao kwa shilingi 120,000 jambo ambalo linawatia unyonge, kwani wao ndio wanaofanya kazi kubwa.

“Mwanzo shirika lilikuwa linanunua kwetu lita moja kwa shilingi laki mbili na wao wanapata faida ya 120,000, lakini kinachotushangaza wamekuja kutushushia bei na wala soko halijashusha bei, hivyo tumepata hasara kubwa na tunadaiwa”, walifafanua.

Mmoja wa wakulima hao Khamis Ramadhan Faraji mwenye shamba lake Mbiji Mkoani alisema, walihamasishwa kulima mchachai, ingawa kwa sasa wameanza kuwavunja moyo kutokana na bei waliyowekewa.

“Sisi ndio tunaofanya kazi kubwa, tunawalipa watu watusaidie lakini kinachotushangaza na kutusikitisha ni kuona shirika wanachukua wao pesa kubwa kuliko sisi wakulima, hii sio haki kutokana na kuwa soko la bidhaa hiyo halijashuka”, alisema mzee huyo.

Alisema, shamba lake lina ukumbwa wa ekari tatu na nusu ambalo huzalisha mafuta mengi baada ya mavuno, ila kinachowasikitisha ni wameanza kuvuliwa matumaini waliyokuwa nayo kutokana na zao hilo.

“Watu ambao niliwaajiri kunisaidia katika shamba langu walinishitaki na kunipeleka mahakamani kwa sababu niliwapa kiwango ambacho hakikufika makubaliano, niliwambia kwamba bei imeshuka lakini hawakunielewa, kwa kweli nilidhalilika mtu mzima”, alielezea.

Aidha alisema, kwa sasa kiwanda ambacho kilikuwa kinawasaidia kukamulia mafuta hayo kimeharibika, jambo ambalo linawarejesha nyuma zaidi kiutendaji, hivyo aliiomba Serikali kuwatengenezea ili kuondokana na changamoto hiyo.

Salma Said Rashid mkulima wa shamba la mchaichai Chonga Wilaya ya Chake Chake alisema, wamekuwa wakipata hasara kutokana na kushuka kwa bei na kukosekana kwa kiwanda cha kukamulia mafuta hayo.

“Tunapata shida wakati tunapotaka kupeleka mchaichai wetu kiwandani, kwa sababu tukipeleka kiwanda cha Mgelema muhusika mkuu anatwambia kiwanda chake ni cha kukamulia majani ya mkarafuu na sio mchaichai na kule Mtakata mafuta hayatoki kwani nyungu zao ni mbovu,” alisema.

Alisema kuwa, walikuwa wanapata faida wao na wananchi wengine, kwani wakinunua mchaimcha katika maeneo tofauti ili kuwasaidia kukuza kipato chao, ingawa kwa sasa wanashindwa.

“Kwa kweli wananchi wengi ilikuwa wanafaidia za bidhaa hii, kwa sababu licha ya kulima sisi pia ilikuwa tunanunua kutoka kwa wakulima wadogo wadogo angalau na wao wakipata kujikwamu kimaisha, lakini kutokana na bei ilivyo sasa tumeshindwa kununua”, alisema Salma.

Asha Juma Rihan mkulima wa mchaichai katika shamba lenye ukubwa wa ekari saba (7) Pujini Pemba alisema, hadi kukamilisha upandaji wa bidhaa hiyo ametumia takribani shilingi milioni 2,000,000.

“Gharama ya ushughulikiaji bidhaa hii ni kubwa sana, mara zote natumia gharama zaidi ya milioni mbili lakini ilikuwa napata faida ila kwa sasa hata gharama hatupati kuzilipa, pia kinachotuumiza zaidi walisubiri tushakamua ndipo wakatushushia bei, hivyo tuliowaajiri hawajui hilo”, alisema.

Hata hivyo, ameiomba serikali kuwaongezea bei wakulima wa mchaichai ili kuimarisha na kuwatia nguvu wakulima wa zao hilo, sambamba na kujipatia faida ambayo itasaidia kuondokana na umasikini.

Mkurungezi Muendeshaji wa Shirika la Biashara Zanzibar la ZSTC Said Seif alisema, shirika lina ulazima wa kununua mafuta ya karafuu na vitu vitokanavyo na karafuu na sio ya mimea mengine, hivyo ikiwa kuna sehemu wanahisi watapata pesa za ziada wakauze midhaa yao.

“Sisi tunanunua pale tunapokuwa na uhitaji na huwa tunauza ujazo mdogo mdogo katika soko la ndani na sio la kidunia, kwa hiyo mkulima ana hiari yake kwenda kuuza ambapo anajua atapata bei kubwa, hawajakatazwa”, alisema.

Alisema kuwa, mafuta ya mchaichai sio ambayo yana soko kidunia ni tofauti na mafuta mengine, hivyo hulisababishia shirika kupata hasara kila mwaka, kwani ununuliwaji wake ni wa kusuasua.

“Iyo bei ya laki tatu sijui wameipatia wapi kwa sababu sisi tunauza kwenye vichupa na sio kwa ujazo huo wanaosema wao, hivyo wanavyosema sio sahihi hata kidogo”, alisema Mkurugenzi huyo.

Hata hivyo Mkurugenzi huyo hakuainisha bei halisi ya kununua mafuta hayo kwa wakulima na kusema kwamba wao huuza kwa soko la ndani kwa ujazo wa vichupa vidogo vidogo na sio ujazo mkubwa.


About mmedia

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment