Tusiwaweke nyuma wanawake twende nao bega kwa bega

Mkurugenzi wa TAMWA-ZNZ Dkt,Mzuri Issa alipokua akizungumza na baadhi ya waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa kuwaunga mkono wanawake katika kampeni zao mbali mbali za kushiriki kwenye uongozi.



Na Salum Vuai

 ZAMA na dahari, katika mila za nchi nyingi za Afrika,   ilikuwa kawaida kumuona mzee wa kiume akienda safari na   mke wake huku yeye akiongoza mbele na mkononi   ameshikilia fimbo na mama akifuata nyuma.

ZAMA na dahari, katika mila za nchi nyingi za Afrika, ilikuwa kawaida kumuona mzee wa kiume akienda safari na mke wake huku yeye akiongoza mbele na mkononi ameshikilia fimbo na mama akifuata nyuma.

Tabia hiyo ilitiliwa nguvu kwa wakati huo ili kuonesha nafasi ya mwanamme kama baba, bwana, kiongozi na msimamizi wa mwanamke iwe katika ngazi ya familia, jamii na taifa kwa jumla.

Aidha katika jamii zinazofuata dini ya Kiislamu, msisitizo zaidi uliwekwa kwa kunasibisha jambo hilo

na dhamana alizonazo mwanamme kwa mujibu wa kitabu kitakatifu cha Kuran, kwamba “Mwanamme ni msimamizi wa mwanamke.”

Tabaan hakuna muumini yeyote wa dini hiyo, awe mwanamke au mwanamme anayepinga ukweli huo, lakini kinachogomba ni ile tabia iliyojengeka miongoni mwa wanaume wengi kutumia mwanya huo kumkandamiza mwanamke.

Kwa kutumia aya hiyo, wapo wanaomuona mwanamke kuwa ni mtu wa kusikiliza na kutii tu amri za mwanamme, awe mumewe au kiongozj katika jamii, na kamwe hana sauti wala haki ya kusikilizwa au kupewa dhamana kubwa hasa ya kiuongozi.

Ingawa sasa kumepigwa hatua kubwa katika kubadilisha mitazamo ya mfumodume na wanawake wameanza kukunjua mbawa pamoja na wanaume na mataifa kuanza kutambua nafasi ya kiumbe huyo mwenye hadhi ya pekee mbele ya Mwenyezi Mungu, bado safari ni ndefu kufikia kilele zaidi cha ufanisi.

Katika hotuba yake aliyoitoa kwenye kongamano la kizazi cha usawa Machi 29, 2021 huko Mexico City, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, alisema; “Miaka 26 baada ya mkutano wa nne wa kimataifa wa wanawake na usawa wa kijinsia, hatua kubwa zimepigwa na mafanikio yameonekana lakini bado dunia inajikongoja kutimiza azimio la Beijing na hatua za kufikia usawa wa kijinsia. 

Kupitia kongamano hilo lililofanyika kwa njia ya mtandao,Guterres alisema; “Wanaharakati wa kutetea haki za wanawake, masuala ya kijinsia na vijana kote ulimwenguni wameendelea kusongesha mchakato wa kufikia lengo la usawa, kuilainisha mifumo dume iliyokita mizizi, kubadili baadhi ya mila na desturi na kuhamisha madaraka na kuwapa wale ambao mara nyingi husahaulika na kunyamazishwa, kumekuwepo na ushindi mkubwa lakini mchakato unakwenda polepole mno na huu ni wakati wa kubadili hilo.” 

Aidha alieleza kuwa, usawa wa kijinsia ni suala la mamlaka ambayo bado yanasalia mikononi mwa wanaume. 

Akaongeza kuwa, katika maeneo mengi, wazo la usawa wa kijinsia limeshambuliwa, sheria za ukandamizaji zimerudi, na unyanyasaji wa kutisha dhidi ya wanawake unaongezeka, mambo ambayo alisema anayalaani kabisa.

Kama hayo hayatoshi, kinara huyo wa UN akaongeza kuwa, mshituko wa janga la COVID-19 nao umeharibu na kusambaratisha maisha ya mamilioni ya wanawake na wasichana na kuathiri hatua za mafanikio mengi yaliyokuwa yamepatikana. 

Na hapa nanukuu kauli ya Guterres: “Huu ni wakati wa kujikusanya na kujipanga tena kwa ajili ya kutimiza azma yetu ya kuunda ulimwengu ulio sawa, wa haki, na endelevu zaidi ambao watu wote wanaweza kutambua haki zao za binadamu bila ubaguzi na bila woga. Na kazi hii ni ya wanawake wote.” 

Hapa Zanzibar na Tanzania kwa jumla, kwa miaka sasa kumekuwa na harakati za kumuinua mwanamke na kutetea haki yake katika masuala mbalimbali ambayo yamekuwa kwa kiasi kikubwa yaking’ang’aniwa na wanaume na kujifanya ndio pekee wenye hakimiliki kwayo.

Kwa upande wa uongozi, demokrasia na nafasi za kutoa maamuzi, mwanamke amekuwa akikumbana na vikwazo vingi zikiwemo sheria kandamizi, na wanaume wengi wamekuwa wepesi kusema eti nafasi ya mama na dada zetu ni jikoni pekee pamoja na kupiga kofi tu pale wanaume wanapogombea nafasi za kuongoza.

Katika tafakuri yake, Muhenga anakazia kwa wino uliokoza wito wa Katibu Mkuu wa UN ambaye alitaja mambo matano muhimu ya kupewa kipaumbele kwa ajili ya kutambua nafasi ya mwanamke.

Mambo hayo ni: 1. Kulinda haki sawa za wanawake na kufuta sheria za kibaguzi. 

2. Kuhakikisha uwakilishi sawa kuanzia katika bodi za kampuni hadi mabunge na zaidi kupitia hatua maalum na nafasi za upendeleo. 

3. Kuongeza ujumuishaji wa wanawake kiuchumi kupitia malipo sawa, ulinzi wa kazi, mikopo inayolengwa na uwekezaji katika uchumi wa huduma na hifadhi ya jamii. 

4. Kuweka mara moja mipango ya hatua za dharura kushughulikia ukatili dhidi ya wanawake na wasichana. 

5. Kutoa nafasi kwa kipindi cha mpito (UVIKO 19),  cha kizazi kinachoendelea na kwa vijana ambao wanatetea ulimwengu ulio na haki zaidi na sawa. 

Kwa muktadha huo, Muhenga anapongeza hatua ya Ubalozi wa Norway hapa Tanzania, kufadhili mradi wa miaka minne visiwani Zanzibar unaohamasisha ushirikishwaji wa wanawake katika masuala ya uongozi, demokrasia na kutanua wigo kwao wa kuingia kwenye vyombo vya kufanya maamuzi.

Mradi huo ulioanza mwaka 2020 chini ya usimamizi wa , TAMWA kwa mashirikiano na ZAFELA pamoja na  PEGAO, ni njia muafaka ya kuwatoa woga wanawake katika kuonesha uwezo walionao na mchango wanaoweza kutoa katika ujenzi wa Tanzania yenye usawa na demokrasia rafiki kwa wote.

Kamwe wanaume wasinune kutokana na ufadhili huu na mingine inayotolewa kwa wanawake, kwani haipo kwa ajili ya kuwapandia kichwani au kuwapoka nafasi na masofa wanayokalia.

Kama tusemavyo, “Kinga na kinga ndipo moto uwakapo, na hawa wanalenga kuunganisha nguvu ili kuleta ustawi zaidi na kuifikia Zanzibar na Tanzania tuzitakazo.

 


About mmedia

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment