Rais Mwinyi ataka ujenzi wa majengo mapya ya Hospital uendane na vifaa tiba



Imeandikwa na Habiba Zarali

Pemba

Rais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema kuwa ujenzi wa majengo ya Hospitali lazima uendane na uwepo wa vifaa tivba vya kisasa.

Hayo aliyaeleza ospitali ya Chake chake, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kuangalia shughuli za maendeleo katika mkoa wa Kusini Pemba sambamba na kuwashukuru wananchi baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Alisema kuwa Serikali itahakikisha kuwa baada ya kumalizika kwa ujenzi huo kuona kuwa vimepatikana vifaa ambavyo vitaweza kuwapatia huduma wananchi wanaofika hapo kwa matibabu sambamba na kuangalia uwezekano wa kujenga majengo mengine ya ghorofa kulingana na eneo lilivyo.

Alisema amefarajika na ujenzi wa Hospitali ya Chake Chake unavyokwenda na kuahidi kutafuta fedha za ziada ili kuona kuwa ujenzi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa.

Alieleza Serikali itaendelea kutatuwa changamoto zinazowakumba watendaji wa Wizara ya Afya ikiwemo stahiki zao lakini aliwasihi kufanya kazi kwa uadilifu wakifikiria kauli mzuri kwa wagonjwa ambayo pekee yake ni tiba.

“Nawaomba wafanyakazi wa Afya muwe na kauli mzuri kwa wagonjwa kwani hiyo yote ni tiba na muelewe kuwa kazi munayoifanya ni ya wito na malipo yake makubwa mutayakuta mbele ya Allah SWT,”alisisitiza.

Hata hivyo aliyakubali maombi ya wananchi juu ya kuongezwa kwa majengo ya ziada baada ya wodi hiyo ya mama na mtoto linalojengwa ili wagonjwa wanaofika hapo wawe na sehemu mzuri ya makaazi.

Akizungumzia suala la kupatikana chakula kwa watu wagonjwa wanaolazwa hospitalini hapo, alisema litaangaliwa ili kuona linafanyika kwa kuwaondolea shida wananchi hususani waliokuwa hawana jamaa karibu.

“Hili la chakula lazima tukae tufikirie bajeti kama inaruhusu kwani sio rahisi kuwapatia chakula watu wote wanaofika hapo, wale ambao wanajamaa wa karibu basi watusaidie kwanza ,”alieleza.

Akitembelea mradi wa maji katika kijiji cha Chanjaani Chake chake Pemba, alisema miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa uhakika ambalo ni suala muhimu kwa wanaadamu.

“ Maji ni uhai na bila ya maji hakuna uhai na tunaona umuhimu wa maji na ndio maana tunafanya haraka ili kuhakikisha huduma hii wananchi munaipata ,”alisema.

Aliiaagiza Mamlaka ya Maji Zanzibar ‘ZAWA’ kuwatengenezea miundombinu ya maji katika sehemu iliopita bara bara ili wananchi waweze kupata huduma hiyo.

Akizungumzia kero ya bara bara Dk. Mwinyi alisema hivi sasa kuna makubaliano na kampuni ya ujenzi wa bara bara hivyo aliwataka wananchi kutoa hofu kuhusiana na suala hilo.

Akikaguwa ujenzi wa bara bara ya Kipapo- Mgelema hadi Wambaa, Dk. Hussein Mwinyi alitowa ahadi kwa wananchi kuwa Serikali itaimaliza bara bara hiyo kwa kiwango cha Lami bila ya kuchelewa.

Katika kuunga nguvu suala la Elimu kwa wananchi wa Mgelema aliahidi kuchangia million 5 kwenye ujenzi wa Skuli ya msingi ambayo wananchi wenyewe wameonesha juhudi ya kuchangishana shilingi 50,000 kwa kila mtu , ili kukamilisha ujenzi huo.

Akipokea maelezo ya ujenzi huo kutoka kwa Daktari dhamana wa Hospitali ya Chake Chake, Abrahman Said Suleiman , alisema kuwa kumalizika kwa jengo la Hospitali hiyo katika wodi ya akinamama na watoto kutaondoa matatizo mengi ikiwepo ongezeko la vitanda kutoka 63 vilivyoko sasa hadi kufikia vitanda 116.

Hata hivyo alisema kuwa Hospitali ya Chake Chake imekuwa ikipokea wagonjwa wengi ikiwa ni ya pili ukiachia ya Mnazi mmoja kwani katika mwezi wa Julai mwaka 2020 hadi Juni 2021 tayari wagonjwa 61,000 walishapatiwa matibabu hospitalini hapo.

“ Kutokana na uwepo wa wagonjwa wengi ni wazi kuwa nafasi ya kuwaweka wagonjwa itakuwa ndogo hivyo baada ya ujenzi huu kukamilika tunaomba na wodi ya akinababa ijengwe kwani kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya watu,”alisema.

Aliomba baada ya kumalizika kwa Wodi hiyo ya akinamama na watoto wanaomba kupatiwa vifaa mbali mbali vya matibabu ikiwemo mashine ya kutambuwa maradhi yasioambukiza na mashine ya Xray.

Alisema hata hivyo kwa sasa wanao madaktari 229 wakiwemo , wataalamu 4 ingawaje kwa sasa hawana sugeon hata mmoja katika Hospitali ya Chake chake.

Kwa upande wake wakala wa usimamizi wa majengo , Mhandisi Nahoda alisema, ujenzi huo hadi kumalizika kwake utagaharimu zaidi ya Shiling bilion moja, ambao kwa sasa tayari umeshafikia asilimia 55 ambao ulianza rasmi Februari 2020 na unatarjiwa kumalizika mwishoni mwa Disemba mwaka huu.

Alieleza kisima hicho kitagharimu shilimngi milion 45 ambapo malengo ya baadae ni kujenga tangi lenye ujazo wa lita million moja ifikapo mwaka 2022.

Dk. Mwinyi anaendelea na ziara yake ya kuangalia miradi ya maendeleo sambamba na kuwashukuru wananchi kwa kumchaguwa kuwa Rais wao ikiwa ni siku ya mwanzo ndani ya mkoa wa Kusini.


About mmedia

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment