
Na Haji Nassor
JUMUIYA ya Utetezi wa Kijinsia na Mazingira Pemba ‘PEGAO imewashauri wanaume kuwafungua pingu za ruhusa na ridhaa wanawake, ili sasa watumie haki yao ya kuwa viongozi, katika sekta mbali mbali.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Ali Mohamed, kwenye mkutano wa wazi, wa uzinduzi wa kamati za kuhamasisha wanawake kudai haki zao za uongozi, demokrasia na siasa, kupitia mradi huo wa ‘SWIL’ unaotekelezwa na PEGAO, TAMWA Zanzibar a ZAFELA uliofanyika uwanja Tenis Chake chake.
Alisema, kwa muda mrefu baadhi ya wanaume wamewatia pingu wanawake na kukosa fursa za kuwa viongozi, huku wanaume hao wakijimilikisha nafasi hizo.
Alieleza kuwa, kila eneo kuanzia kwenye familia, kamati za vijiji, mitaa, wilaya, jimbo, mkoa na taifa nafasi za juu zimekuwa zikioongozwa na wanaume, jambo ambalo liliimarisha mfumo dume.
“Sasa ni wakati sisi wanaume kuwafungua pingu wanawake na ili wapate hamu nao saa kuwa viongozi, katika kamati za maendeleo, sacos, shehia, wilaya, mkoa na taifa, maana katiba na sheria hazijawabagua,’’alifafanua.
Hata hivyo Mwenyekiti wa huyo wa PEGAO, amekipongeza chama cha waandishi wa habari Wanawake Tanzania TAMWA-Zanzibar, kwa kutafuta mradi huo wa Kuwawezesha wanawake kudai haki zao za kisiasa, kidemokrasia na uongozi ‘SWIL’ ambao unalenga kuwafikia wanawake 6,000.
Mapema Mratibu wa mradi huo kutoka TAMWA-Zanzibar Salma Amir Lusangi, alisema mradi huo haulengi tu kuwahamasisha wanawake kuingia kwenye nafasi za uongozi za kisiasa pekee, bali kila sekta.
Alisema, haipendezi kuona kwenye sacos, kamati ya shehia, familia, kamati za majimbo, wilaya, mkoa na taifa nafasi za juu zinashikiliwa na wanaume pekee.
Alifafanua kuwa, ili kulioandoa hilo, na ndio tasisi hizo za PEGAO, TAMWA-Zanzibar na ZAFELA zinafanyakazi pamoja, ili kuona azma ya mradi huo zinafikiwa.
“Kwenye mkutano huu wa wazi hapa Tenis Chake chake, ni sehemu ya utekelezaji wa mradi, na tunazindua kamati ya wananachi ‘citizens brigade’ ambayo hii itafanya kazi ya kuwahamasisha na kuwaelimisha wanawake kudai haki zao za uongozi,’’alifafanua.
Kwa upande wake Mratibu wa huo kutoka Jumuiya ya Utetezi wa Kijinsi na Mazingira Pemba ‘PEGAO’ Dina Juma Makota, alisema ili kufikia malengo hayo, jamii haina budi kuwaunga mkono.
Mkurugenzi Mtendaji wa ‘PEGAO’ Hafid Abdi Said, alisema inawezekana mno, kufikia usawa wa kijinsia wa 50 kwa 50 kati ya wanawake na wanaume kwenye safu ya uongozi.
Alisema jumuiya yake, imepania mno na hasa kupitia mradi huo wa ‘SWIL’ unaoendeshwa kati yao na TAMWA-Zanzibar na Jumuiya ya Wanasheria wanawake Zanzibar ZAFELA.
“Hapa tunachoomba ni jamii na hasa kundi la wanaume kutuunga mkono, ili sasa kumtoa mwanamke naye kushika hatamau za uongozi, kuanzia ngazi ya familia hadi taifa,’’alifafanua.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Katibu tawala wilaya ya Chake chake Omar Juma Ali kwa niaba ya Mkuu wa wilaya hiyo, alisema historia inatosha, kuonesha jinsi mwanamke alivyokosa thamani miaka kadhaa iliyopita.
Alisema, hakuoenekana na thamani yoyote katika familia, jamii na taifa lake, na kusababisha kuendelea kuwakilishwa hata kwa mambo yanayomuhusu moja kwa moja.
Alieleza kuwa, hilo liliwadumaza na kukosa kujiamini, na kuwaacha wanaume wakidhani kuwa, ndio wenye haki miliki ya kushika madaraaka.
“Lakini leo hii niipongeza TAMWA- Zanzibar, imekuja kuwazindua wanawake na wenye mamlaka, kuwa hakuna sheria, maazimio wala katiba inayomkataza mwanamke kushika uongozi,’’alifafanua.
Hata hivyo alisema miradi kadhaa inyoendeshwa na TAMWA-Zanzibar, imekuwa ikilenga kuwaonesha haki na fursa zao wanawake, na kilichobakia kwa jamii ni kubadili tabia.
Muhamasishaji wa kutoka timu ya wananchi ‘citizens brigade’ Safia Saleh Sultan, alisema bado zipo changamoto kwa wenye mamlaka, kwa kumtazama tofauti mwanamke kwenye uongozi.
Baadhi ya wananchi walisema wakati umefika kwa jamii kubadilisha mtazamo kwa wanawake, na hasa kwa vile katiba na sheria hazijawabaugua.
Aliyewahi kugombea nafasi ubunge wa Jimbo la Chake chake Fatma Dotto Shauri, alisema kwa chama alichoamua kugombea, alivunjwa moyo na wapiga kura.
Mradi wa kuwajengea uwezo wanawake kudai haki zao za demokrasia, siasa na uongozi unaofadhiliwa na Ubalozi wa Norway, unatekelezwa na Jumuiya ya Utetezi wa Kijinsia na Mazingira Pemba ‘PEGAO’ TAMWA Zanzibar kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar ‘ZAFELA’.
Mwisho
0 Comments:
Post a Comment