![]() |
| waziri Mkuu wa Tanzania Kasim Majaaliwa |
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema muswada wa Bima ya Afya kwa
wote utakapokamilika utakuwa ni mkombozi mkubwa kwa Watanzania kwani
utakwenda kufanikisha mkakati wa Serikali wa kuwapatia watanzania huduma bora za
afya.
Amesema Serikali inaendelea kufanya maboresho makubwa ya ujenzi
wa miundombinu ya afya, zikiwemo hospitali pamoja na vifaa tiba, hii ikiwa ni
dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya na
zenye uhakika.
“Serikali inaimarisha upatikanaji wa bidhaa
za Afya nchini ikiwa ni pamoja na dawa, vifaa tiba na kuanzia mwezi Juni,
Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 31 kwa ajili ya
kuhakikisha vifaa hivyo vinapatikana hivyo nataka niwahakikishie watanzania
kuwa Serikali itaendelea kuimarisha hali ya upatikanaji wa dawa na huduma bora
za afya nchini” Alisema.
Waziri Mkuu Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Septemba 25, 2021)
wakati akizungumza na wananchi waliojitokeza kushiriki mbio za hisani
zilizoandaliwa na benki ya NMB
Amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa
Samia Suluhu Hassan imeanza ujenzi wa kiwanda kwa ajili ya uzalishaji wa
‘Gloves’ na dawa aina tano zikiwemo vidonge, ‘syrup’, ‘Capsules’, kwa lengo la
kukidhi mahitaji ya nchi.
“Kiwanda hicho kitasaidia kuokoa shilingi bilioni 33
ikilinganishwa na shilingi bilioni 54 kwa mwaka ambazo zinatumika kununua
bidhaa za afya sita zitakazozalishwa kiwandani hapo”
Aidha, Waziri Mkuu ametoa pongezi kwa benki ya NMB na CCBRT kwa
pamoja na wadau wengine kwa namna wanavyounga mkono Serikali katika kuwahudumua
kinamama wanaopata ugonjwa wa Fistula
Naye, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Dkt. Doroth Gwajima amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano wanawake zaidi
ya elfu tano miatano wameshatibiwa ugonjwa wa fistula na asilimia kubwa
wametibiwa katika Hospitali ya CCBRT.
“Hii inatokana na kampeni ya inayoendeshwa kati ya Serikali na
wadau ambao kuna mabalozi zaidi ya 3000 nchi nzima kushughulikia wagonjwa wa
fistula na kuwapeleka katika hospital zinazotoa huduma za fistula.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB Ruth
Zaipuna amesema kuwa lengo la mbio hizo zilikuwa ni kukusanya fedha kwa ajili
ya wanawake wanaosumbuliwa na ugonjwa wa fistula.
Zaipuna amesema kuwa, kupitia mbio hizo za hisani wamefanikiwa
kukusanya kiasi cha Shilingi milioni 400 ambao zitaweza kutoa matibabu kwa
kinamama 100 wanaosumbuliwa na ugonjwa wa Fistula.

0 Comments:
Post a Comment