Mke wa Makamu wa kwanza ataka elimu zaidi itolewe kwa jamii dhidhi ya watu wenye ulemavu

 


Imeandikwa na Haji Nassor,Pemba

hnasor@marhabanews.net


MKE wa Makamu wa Kwanza wa rais Zanzibar, Mama Zainab Kombo Shaib amesema, bado elimu inahitajika kwa jamii, ili kundi la watu wenye ulemavu, lipate nyenzo ambazo zitawawezesha kumudu maisha yao na kuacha utegemezi.

Alisema, bado elimu ya kutambua jambo hilo iko chini, na waliowengi wanadhani kuwa kundi la watu wenye ulemavu halina nafasi ya kushawishi maendeleo katika maeneo yao.

Mke huyo wa Makamu wa Kwanza aliyasema hayo leo Augusti 7, mwaka huu, kwenye mkutano wa kujadili umuhimu wa kuandikwa kwa habari za watu wenye ulemavu, ulioandaliwa na Internews kupitia njia ya kielektroniki ya ‘zoom’.

Alisema watu wenye ulemavu hukabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo kukumbwa na magonjwa na kisha kushindwa kupata matibabu kutokana na kuzidiwa na umaskini wa kipato.

Alieleza kuwa, wapo wengine wanaopata ulemavu kutokana na ajali, na kisha matibabu tokea asili huwa magumu jambo linalopelekea kukatwa moja ya viungo vyake na kupata ulemavu.

“Jamii inahitaji kupata elimu ya kuwatambua watu wenye ulemavu, ili kwanza kwa wale wanaozaliwa wakiwa na mashaka ya viungo vyao, wapatiwe matibabu haraka,’’alieleza.

Katika hatua nyingine, Mke huyo wa Makamu wa Kwanza, alifafanua kuwa, ulemavu unaosababishwa na maradhi au ajali unaweza kuepukika, ikiwa watendaji watawajibika ipasavyo kimatibabu.

Aidha aliitaka jamii, kuacha kuwanyanyapaa watu wenye ulemavu, kwani kila mmoja ni mlemvu mtarajiwa, hivyo ni vyema akaishi kweye kundi la kimaadili kabla ya kuingia moja kwa moja.

“Lakini niwapongeza sana shirika la Internews Tanzania kwa kuwawezesha waandishi wa habari wa Tanzania bara na visiwani na kusababisha kuibua watoto waliotelekezwa kutokana na ulemavu wao,’’alifafanua.

Akifungua mkutano huo, Mkuu wa kanda wa miradi kutoka Shirika la Internews nchini Kenya Jackie Lidubwi, amesema kazi inayofanywa na waandishi wa habari, inaweza kuleta mageuzi makubwa kwa watunga sera, ili kundi la watu wenye ulemavu lipate haki zao stahiki.

Alisema Internews liliendesha mafunzo maalum kwa waandishi wa habari, kwa lengo la kuhakikisha wanakuwa waledi katika uandishi na utengenezaji wa vipindi.

Hata hivyo, alisema kazi hiyo inafaa kuendelezwa, kwani kazi ya waandishi wa habari huwa ni ya kudumu ili kuona makundi kama hayo yanapata haki zao.

Mapema Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Nipashe Beatrice Bandawe, alisema sasa chombo chake kimeamka na kuandika habari 20 za watu wenye ulemavu kwa mwezi.

“Kabla ya mimi kupata mafunzo na waandishi wetu juu ya kuandika habari za watu wenye ulemavu, hatukuwa tukizalisha habari hata 5 kwa kwezi, lakini sasa zinafika 20 ni jambo la kujivunia,’’alieleza.

Mwandishi aliyepata mafunzo hayo ya kuandika habari za watu wenye Ulemavu na kuwezeshwa na Internews, kutoka kituo cha redio cha CGFM Vivian Pyuza , alisema habari ya mtoto aliyetekezwa na familia, imesaidia na sasa anataka kupatiwa haki yake ya elimu.

Mkuu wa Programu, Shirika la Vijana wenye Ulemavu Genarius Ernest Gaisha, (YoWDO) alisema vyombo vya habari vinaendelea kufanya kazi nzuri ya kuibua changamoto kwa kundi la watu wenye ulemavu.

“Mfano tovuti ya pembatoday imeripoti habari ya Afisa Mdhamini kukemea udhalilishaji kwa watu wenye ulemavu, au mitandao ya kijamii imewafichua watoto wenye ulemavu walivyofichwa,’’alieleza.

Kwa upande wake Mtendaji kutoka Afisi ya Waziri Mkuu Josephine Lyengi, alisema hali za watu wenye ulemavu kwa sasa imeimarika ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

“Miundombinu ya majengo ya umma sasa yamefuata urafiki kwa kundi la watu wenye ulemavu, ukiachia yale majengo yaliyojengwa zamani,’’alieleza.

Wakichangia mada kwenye mkutano akiwemo Mhariri wa kituo cha Redio cha Hits Fm Zanzibar Salmin Juma, alipendekeza kila jengo la umma lazima lizingatie mazingira rafiki ya watu wenye ulemavu.

Mhariri wa habari wa Gazeti la Zanzibar leo Zanzibar Juma Khamis Juma, alisema kazi iliyofanywa na waandishi wao waliowezeshwa na Internews, imeibua changamoto kadhaa kwa kundi la watu wenye ulemavu.

Akifunga mkutano huo Mratibu wa miradi kutoka Internews Shaaban Ramadhan Maganga aliwasukuru washiriki, na kuwataka waendelee kufanya kazi hata kama mradi huo umemalizika.

Hata hivyo amewataka wahariri kuwahimiza waandishi wao wote, kuandika habari za watu wenye ulemavu, ili liishi kama makundi mengine ndani ya jamii.

“Endeleeni kulipa hadhi na nafasi ya pekee kundi la watu wenye ulemavu, ili lipaze sauti zao na kupata maisha bora baada ya kupata haki zao,”alifafanua.

Mwisho

About mmedia

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment