
Na Haji Nassor,Pemba
Katika hali isiokua ya kawaida kwa wazazi hatimae Mahakama ya watoto Mkoa Chake chake Pemba, imeridhia ombi na kisha kuwanyang’anya mke na mume wanywaji pombe, mtoto wao wa miezi mitatu, kutokana na kumtekeleza wanapokwenda kwenye starehe zao.
Umuzi huo umetolewa na Hakim wa mahakama hiyo, Luciano Makoye Nyengo, Augusti 2, mwaka huu, kufuatia lalamiko lililowasilishwa mahakamani hapo, na Idara ya Hifadhi ya mtoto wilaya ya Chake chake.
Ombi hilo, liliwasilisha mahakamani hapo mwishoni mwa mwezi uliopita, likidai kuwepo kwa mke na mume wakiendelea kumtelekeza mtoto wao wa miezi mitatu.
Kwenye ombo hilo, lililosainiwa na Afisa wa Idara ya Hifadhi ya mtoto wilaya ya Chake chake Rashid Said Nassor, alisema wazazi hao, baada ya kurudi kwenye starehe zao, wamekuwa wakimtekeleza mtoto wao.
“Wazazi hao wanaotumia pombe, wakirudi wamekuwa wakimpiga na wakati mwengine huvutia kama nguo, jambo lingeweza hata kumsababishia mauti mtoto huyo,’’alisema.
Ombi hilo, lilizidi kueleza kuwa, tabia hiyo imekuwa endelevu na hata wakati mmoja, jirani kumuoko mtoto huyo, baada ya kuangushwa na wazazi na kupoteza fahamu.
Hivyo, Afisa huyo aliiomba mahaka kutoa uamuzi wa mtoto huyo, kuondolewa kwenye ulezi wa wazazi wake wa asili, na kukabidhiwa Idara ya Hifadhi ya mtoto, kwa ajili kumpatia haki yake ya malezi.
“Mtoto ana haki zake kadhaa, ikiwemo moja baada ya kuzaliwa ni kulelewa kimaadili ili akue kwenye malezi ya tabia njema, lakini kwa huyu hatofikia hayo, maana wazazi wake wamekuwa wakimtelekeza,’’alifafanua.
Baada ya Mahakama ya watoto mkoa Chake chake kupokea ombi hilo na kujiridhisha, iliamua kuwa, mke na mume huyo kunyang’anywa mtoto wao na kuwaacha wao kuendelea na starehe zao.
“Kuanzia leo Augusti 2, mwaka huu Mahakama imeamua mtoto huyo asilelewe na wazazi wake, kutokana na kubainika kumtekeleza mara baada ya wao kunywa pombe, jambo linamuhatarishia usalama wake,’’alisema.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mara baada uamuzi huo wa mahkama, Afisa Hifadhi ya mtoto wilaya ya Chake chake Rashid Said Nassor, alisema ameupokea kwa furaha uamuzi huo.
Alisema, anachoamini kuwa mahakama imetendea haki mtoto huyo, kwani kwa umri wake hakupaswa kutenganishwa na wazazi, lakini ikibidi na ikibainika hawana malezi, kupokonywa ni jema zaidi.
“Awali tulipokea taarifa kutoka kwa Mratibu wa wanawake na watoto wa shehia ya Mgogoni wilayani humo, akiripoti juu ya madhila, dhiki na ukatili anaoupata mtoto huyo,’’alifafanua.
Alisema, baada ya hapo waliweka mtego na wakati wanakwenda kwenye starehe zao za ulevi, na kumuacha ndani mtoto huyo peke yake, alichukuliwa na kufikisha kituo cha Polisi Madungu Chake chake.
Kwa upande wake Afisa wa Idara ya Ustawi wa Jamii wilaya ya Chake chake Omar Mohamed Ali, alisema baada ya hapo walifungua maombi mahakama ya watoto, juu ya wazazi hao kunyannga’anywa mtoto huyo.
“Mtoto kisheria hutakiwa kulelewa na wazazi wake, lakini ikionekana wenyewe hawana malezi, hakuna budi sisi kuingilia kati kisheria, ili kuyaokoa maisha ya mtoto husika,’’alisema.
Alisema baada ya uamuzi wa mahakama, sasa mtoto huyo amekabidhiwa kwa babu yake mzaa mama, anaeishi Chanjaani wilaya ya Chake chake.
“Makabidhiano ya mtoto huyo yalifanyika chini ya Idara ya Ustawi wa jamii, Idara Hifadhi ya mtoto na Jeshi la Polisi na sasa analelewa na babu yake na bibi,’’alieleza.
Taarifa zilitolewa na majirani ya wazazi hao, zinaeleza kuwa familia hiyo, ambyo imeshapata watoto watano, wote wameshanyang’anywa kutokana na tabia zao mbaya.
“Watoto wao wanne wako kwenye skuli zenye dakhalia mbali mbali za Zanzibar na Tanzania bara, kwa kule kuwatelekeza baada ya kumaliza kunywa pombe,’’alieleza.
Walipopigiwa simu wazazi hao Salma Said Massoud na mume wake Abdalla Mohamed wakaazi wa Mgogoni, hawakutoa ushirikiano.
Mwisho
0 Comments:
Post a Comment