Mahakama Pemba yampelekea Chuo cha Mafunzo aliemkata mwenzake kiganja kwa wivu wa mapenzi



Na Haji Nassor,Pemba


Mahakama  ya Mkoa Chake chake, imemtupa chuo cha mafunzo kwa muda wa miaka 14, mshitakiwa Abdulla Ahmada Mohamed wa Gongomawe Chanjaani Chake chake, baada ya kupatikana na hatia ya kumshambulia kwa panga na kumkata kiganja, mtu aliyeamdhania kumchukulia mke wake.

Mahakama hiyo chini ya hakimu Luciano Makoye Nyengo, pamoja na adhabu hiyo, ilimtaka mshitakiwa huyo kumlipa muathirika fidia ya shilingi milioni 1, kutokana na maumivu aliyoipata na kupoteza kiungo.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, ilifahamika mahakamani hapo kuwa, mshitakiwa huyo alimpiga panga muathirika baada ya kumuona tu, akitoka ndani mwake, akidai amekuwa na tabia ya kumchukulia mke wake.

Ilifahamika mahakamani hapo kuwa, mshitakiwa huyo alidai muathirika huyo kabla ya kumshambulia kwa panga, amekuwa na utamaduni wa kutumia nguvu kuingia ndani ya nyumba yake na kwa dhamira ya kutenda kosa.

Ilielezwa kuwa, mshitakiwa huyo aliadai ndipo siku moja wakati anatoka safari zake, alipomuona mshitakiwa akitoka ndani ya nyumba yake na kuamua kumshambulia kwa panga.

Hakimu wa mahakama hiyo kabla ya kutoa uamuzi huo, alisema kuwa muathirika huyo alishambuliwa sehemu mbali mbali za mwili wake, ikiwa ni pamoja na mdomoni, kichwani na mkono wake wa kulia.

“Kutokana na mshitakiwa kumuathiri vibaya muathirika, baada ya kufikishwa hospitali, ilibadi mkono wake kuanzia kwenye kisugudi ukatwe, na sasa anaishi na mkono mmoja,’’alisema hakim Luciano.

Alisema kwenye shauri hilo ambalo kwa mara ya kwanza lilipanda kizimbani Disemba 23, mwaka jana, jumla ya mashahidi tisa walitoa ushahidi wao makahamani hapo.

Mmoja wamashahidi hao daktari katika hospitali ya Chake chake, alithibitisha kumpokea mjeruhiwa huyo, akiwa na hali mbaya, kutokana na kushambuliwa huko.

“Ni kweli Disemba 13, mwaka jana nikiwa kazinini hospitali ya Chake chake, alifika mutahirika akiwa anavuja damu sehemu zake mbali mbali, na kisha kumuhudumia,’’alisema daktari huyo.

Aidha muathirika huyo wakati akitoa ushahidi wake, alisema kuwa alishambuliwa na mshitakiwa Abdulla Ahmada Mohamed kwa panga na kumsababishia maumivu makali.

“Kutokana na alivyonishambulia ilibidi mkono wangu wa kulia ukatwe hospitali, maana vyenginevyo ningekuwa na athari mbaya zaidi,’’alifafanua.

Baada ya mashahidi hao kutoa usahidi wao kwa nyakati tofauti, siku ya mahakama kupanga hukumu hiyo, ilifika mahakamani hapo.

Kabla ya hukumu hiyo, Mwendesha Mashtaka kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Ali Amour Makame, aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kweke, ili iwe fundisho na kwake kwa wengine wenye tabia hiyo.

“Makosa ya kujichukulia sheria mikononi katika jamii yamekuwa yakijitokeza siku hadi siku, hivyo naiomba mahakama hii tukufu, kumpa adhabu kali mshitakiwa ili na wengine waingie woga,’’alisema.

Ndipo Hakimu Luciano Makoye Nyengo alipotumia kifungu cha 204 (a) cha sheria ya Adhabu nambari 6 ya mwaka 2018 sheria ya Zanzibar, kumtia hatiani mshitakiwa huyo.

Awali ilielezwa kuwa Disemba 12, mwaka jana majira ya saa 7:30 mchana eneo la Gongomawe Chanjaani, wilaya ya Chake chake, kwa maksudi mshitakiwa huyo, alimshambulia kwa panga Issa Khamis Massoud miaka 48.

Alidai kufanya hivyo, kwa madai ya mwenendo wa Issa (muarithika) kuingia ndani mwake kwa nguvu na kisha kuendesha tendo la ndoa la kulazimisha na mke wake, ambapo haki ya rufaa imetolewa kwa asiyeridhika na uamuzi huo.


Asante kwa kutembelea tovuti hii,sasa tumekurahisishia kupata habari mbali mbali kwa njia ya haraka zaidi cha kufanya ingia play store kisha andika jina marhaba news na download  au fungua link hii hapa https://play.google.com/store/apps/details?id=iot.net.marhabanews

About mmedia

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment