| Baadhi ya wanufaika wa mradi wa Viungo kutoka shehia ya Donge Mkoa wa kaskazini Unguja wakiendelea kuania mboga kwa ajili ya usindikija katika mafunzo hayo. |
| Mkufunzi kutoka mradi wa Viungo Salma Nassor Marshed (Mwenye mtandio mwekundu) akiwafahamisha wanufaika wa mafunzo hayo jinsi ya kusindika nyanya zisiweze kuharibika. |
Wanufaika wa mradi wa VIUNGO visiwani Zanzibar
wameanza kupatiwa mafunzo ya usindikaji wa mboga mboga na uongezaji wa thamani
kwa bidhaa wanazozalisha,ikiwa ni awamu ya kwanza ya mafunzo hayo ya usindikaji
kupitia mradi huo.
Utolewaji wa mafunzo hayo umekuja ikiwa ni sehemu ya
utekelezaji wa mradi kwa lengo la kuwajengea uwezo wanufaika wa mradi kujijenga
zaidi kiuchumi ikiwemo kuanzisha biashara kutokana na mazao wanayozalisha.
Akitoa mafunzo hayo Afisa kilimo kupitia mradi wa
Viungo Salma Nassor Marshed alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha
wakulima kusindika mazao yao ili kukabiliana na uhaba wa masoko na kwamba sasa
wataweza kuhifadhi mazao hayo bila kuharibika.
Alisema usindikaji huo pia utaongeza lishe kwa akina mama
na watoto kwani wataweza kutumia mboga mboga zilizosindikwa hata wakati wa kiangazi.
Sambamba na hayo alisema usindikaji huo pia utaongeza
thamani ya fedha kwani mkulima ataweza hifadhi bidhaa alizosindika hata wakati
wa kiangazi ambao matunda na mboga nyingi huadimika.
Kwa upande wake Afisa lishe kupitia mradi huo Witness
William alisema mafunzo ya usindikaji wa mboga mboga yatawafikia walengwa zaidi ya elfu tano kutoka
wilaya kumi za mradi VIUNGO Unguja na
Pemba.
Alisema wanufaika wa mafunzo hayo watakua na jukumu la
kuwafundisha wengine ili walio wengi zaidi waweze kunufaika na elimu hio kwa
maslahi ya wote.
Akifafanua kuhusu umuhimu wa usindikaji alisema wanufaika
wataweza kuimarisha afya za familia zao, sambamba na kukuza kipato chao kwa
kuingiza fedha zitakazotokana na mauzo ya bidhaa zao.
Kwa upande wao baadhi ya wanaufaika wa mafunzo hayo
walisema yamekuja wakati sahihi ambao wakulima wengi walikosa njia sahihi za
kuhifadhi mazao yao.
Walisema kwa muda mrefu wamekua wakishindwa kufahamu
njia bora za usindikaji wa mazao na kufanya kilimo chao kuwa cha muda maalumu
na pindi wakati wa kiangazi unapofika hawakua na hata hakiba ndogo ya mboga
mgoga na matunda.
Mradi huu wa Viungo visiwani hapa unatekelezwa na PDF
kwa mashirikiano ya TAMWA-ZNZ pamoja na CFP chini ya ufadhili wa umoja wa Ulaya
kwa muda wa miaka minne.
0 Comments:
Post a Comment