Elimu humuongezea mtu maarifa na ujuzi wa kuitawala kazi yake, na hivyo kuweza kuifanya bila kusimamiwa ambapo mwishowe matunda huonekana na kumfurahisha mwajiri.
Elimu humpandisha hadhi mfanyakazi na kumfanya aaminike na mamlaka za nchi, hivyo kuwekwa kwenye orodha ya watumishi wanaotegemewa kukabidhiwa dhamana nyengine kubwa inapohitajika.
Kwa kuutambua umuhimu wa elimu, inafurahisha kuona wafanyakazi wengi katika sekta ya umma wakihamasika kutafuta nafasi za masomo ya juu katika vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Hali hiyo imeiwezesha nchi kuzalisha watumishi wengi waliofikia kiwango cha juu cha elimu kama vile, shahada ya kwanza na ya pili, uzamivu na hata uprofesa na ambao wamekuwa tegemeo kubwa kwa taifa katika ubunifu wenye tija.
Miongoni mwa hao, wapo ambao hawakuwa wamefaulu mitihani ya taifa ya kidato cha tatu ambacho miaka ya nyuma ilikuwa ndio ukomo wa elimu ya lazima, lakini hawakukata tamaa wakaamua kujiendeleza hadi sasa kuwa wabobevu wa taaluma mbalimbali.
Hawa walijiendeleza wakiwa kazini na kufanikiwa kujiongeza thamani kwa waajiri wao na serikali, na hatimaye kuwa watu wa kutegemewa na taifa.
Na haya wasingeweza kuyafikia kama wasingepata ushirikiano wa wakuu wao wa kazi ambao kimsingi, wanapaswa kuwapa moyo watumishi wenye hamu ya kujiinua kielimu.
Lakini katika hali isiyopendeza, kuna baadhi ya wakuu wa kazi katika baadhi ya taasisi ambao ni kikwazo na huamua kuwakwamisha bila sababu za msingi watumishi wanaotaka kusaka elimu na mafanikio zaidi.
Mathalan, mfanyakazi ameomba nafasi ya kusoma katika chuo cha hapa nchini au nje akitarajia ofisi yake itambeba kwa kulipia gharama za masomo, lakini anakumbana na danadana zisizokwisha ambazo mtu akiziangalia kwa makini atajua kwamba lengo ni kumuangusha makusudi.
Hiyo si dhana bali ni ukweli kwani ziko taasisi zenye ukwasi mkubwa na hazishindwi kupata fedha za kumsomesha mtumishi lakini zinaamua tu kumkandamiza sijui kwa faida ya nani.
Lakini wakati huohuo na katika taasisi hizo hizo, wapo wafanyakazi wanaolipiwa masomo hata kwa kufululiza, mathalan akimaliza shahada ya kwanza tu anaingiziwa fedha kuunganisha ya pili yaani ‘Master degree’ huku wengine wakililia angalau kusoma stashahada lakini wanakosa mliwazi.
Tatizo hilo halipo kwa upande wa wanaotaka kusoma tu, bali hata wafanyakazi wanaoomba uhamisho kwenda katika taasisi nyengine ambazo pia ni za serikali ili waweze kuinuka kimaslahi, nao huhenyeshwa hadi kukata tamaa.
Wapo baadhi ya wafanyakazi wa sekta ya umma ambao kutokana na taaluma yao kutotumika vyema na kushindwa kunufaisha pahala walipo, hubahatika kutakiwa katika taasisi nyengine zilizoona thamani yao lakini kukubaliwa kuondoka inakuwa shida sana.
Mtu anaporudi kutoka chuoni baada ya kuongeza utaalamu, matarajio yake ni kuona mabadiliko kimaslahi na kustawisha maisha yake, na kama hayapati ndipo anapoamua kujitafutia sehemu nyengine ili naye ainuke kama walivyo mabosi wanaomuwekea ‘kauzibe’.
Tafakuri ya Muhenga inapenda kuzishauri taasisi zisizojua faida ya wasomi, zisione shida kuwafungulia milango kwenda kule watakothaminiwa ambako pengine pia ni sekta ya umma na wataitumikia na kuinufaisha Zanzibar hii hii.
Kuendelea kuwang’ang’ania watumishi wenye ujuzi lakini mkashindwa kuwatumia ipasavyo, ni sawa na tabia ya ‘joka la mdimu’ ambalo hukaa chini ya mti huo kuzuia wanaohitaji ndimu ambazo yeye hana haja nazo. Tubadilike.
Simu: 0777 865050/0714 425556
Baruapepe: salumss@yahoo.co.uk

0 Comments:
Post a Comment