
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema zinahitajika nguvu za pamoja kutoka kwa viongozi wote wa serikali duniani na kwa haraka sana ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoikabili dunia.
katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo mjini New York, Marekani Guterres amesema, ripoti iliyotolewa mapema hii leo na jopo la wataalamu wa mabadiliko ya tabianchi IPCC imeonesha shughuli za kibinadamu zinazidi kuiathiri sayari dunia na joto limezidi kuongezeka ilihali kuna makubaliano yaliyofanyika Paris ya nchi zote kupunguza gesi ya ukaa.
“Ripoti ya leo ya IPCC imeonesha alama ya hatari, shughuli za kibinadamu zinaendelea kuathiri dunia na haziwezi kukanushwa kwani kuna ongezeko la uzalishaji wa gesi ya ukaa, ukataji wa miti na shughuli zote hizi zinawaweka mabilioni ya watu katika hatari. Joto limeathiri kila kona ya dunia na mabadiliko mengi hayatabiriki.”
Akizungumzia mkabata wa kukabiliana maarufu kama mkataba wa Paris Guterres amesema, “kwa sasa tupo kwenye nyuzi joto digrii 1.2 Celsius na joto lingali likiongezeka kwa haraka huku viwango vya gesi chafu navyo vikiongezeka, hali mbaya ya hewa na majanga mengine pia yakiongezeka. Kizingiti tulichokubaliana kimataifa cha joto digrii 1.5 celsius kiko karibu sana kufikiwa na hii ni hatari na lazima tuchukue hatua sasa.”
Kila mtu yupo hatarini
Ripoti ya jopo la wataalamu wa mabadiliko ya tabianchi -IPCC imeonesha shughuli za kibinadamu zinazotokana na uzalishaji wa hewa ya ukaa zimechochea kuathiri hali ya hewa kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea katika miaka 2000 iliyopita.
Iwapo kiwango cha joto kitaendelea hivyo bila kudhibitiwa, itakuwa na madhara mabaya mno kwa binadamu, kwa ekoloji na kwa uchumi, na kusababisha uhaba wa chakula, majanga ya moto kuongezeka, kuongezaka kwa kina cha bahari na kusababisha hali mbaya mno ya hewa.
Fedha zilizopangwa kutolewa ili kusaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zimetolewa asilimia 21 pekee. Hivyo makampuni ya uwekezaji na mabenki yamehimizwa kuwekeza katika shughuli zinazolenga kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi angalau kwa asilimia 50 huku kipaumbele kikisisitizwa kutolewa kwa makundi yenye uhitaji zaidi ikiwemo wanawake na watoto.
Uzalishaji wa gesi ya ukaa usipopunguzwa kwa asilimia 7.6 kila mwaka kati ya 2020 na 2030, dunia haitaweza kufikia nyuzijoto 1.5 za kiwango cha joto zinazolengwa kufikiwa chini ya Mkataba wa Paris
Nini suluhisho?
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametoa mapendekezo kadhaa ya kukabiliana na hali hii ambayo ni;- dunia kuhakikisha ina uchumi wa kijani, kuna juhudi za makusudi kuhakikisha kuna hewa safi na nchi tajiri pamoja na mashirika makubwa ya kimataifa, kujiunga na umoja wa kutozalisha hewa ya kaboni.
Pia amesisitiza nchi hizo tajiri au G20 kuimarisha na kutimiza ahadi zao kwa kutoa michango na kuweka sera zinazokubalika kimataifa kabla ya mkutano wa kimataifa wa masuala ya hali ya hewa wa Umoja wa Mataifa unatarajiwa kufanyika huko Glasgow, Scotland baadae mwaka huu 2021.
“Nchi za OECD lazima zimalize makaa ya mawe yaliyopo ifikapo mwaka 2030, na zingine zote zifuatazo ifikapo mwaka 2040. Nchi zinapaswa pia kumaliza utafutaji na uzalishaji mpya wa mafuta na kutafuta na kutoa ruzuku kwenye mafuta mbadala. Kufikia 2030, kuwe na uwekezaji mara nne zaidi kwenye umeme wa jua na upepo na uwekezaji wa nishati mbadala mara tatu zaidi.” amesema Guterres
Utunzaji wa misitu, maeneo oevu, na mifumo mingine ya ekolojia ni muhimu katika kukabiliana na hali mbaya ya hewa, kutunza makazi, mimea, usambazaji wa maji na miundombinu. Kuhifadhi na kuboresha mifumo hii muhimu ya ekolojia kutasaidia kukabiliana na changamoto zilizopo hivi sasa katika sayari dunia.

0 Comments:
Post a Comment